WASABATO WAISHINDA SERIKALI MAHAKAMANI



Kanisa la Waadventista Wasabato leo limeishinda serikali katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mwalimu Ezekiah Oluoch dhidi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Mazingira na Muunguno, January Makamba pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Katika shauri hilo Mwalimu Ezekiah alikuwa akipinga muongozo wa Waziri huyo unaotaka kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa siku maalumu ya kufanya usafi kitaifa. Mwalimu huyo alidai kwamba agizo hilo la serikali linaingilia haki na uhuru wa kuabudu kwa Wakristo wa madhehebu ya Waadventista Wasabato, ambao kwa imani yao siku ya jumamosi hawatakiwi kufanya kazi.



Mwalimu Oluoch aliiomba mahakama, pamoja na mambo mengine, itamke kwamba agizo hilo la kufanya usafi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi linaingia uhuru wa kuabudu kwa waadventista wasabato.



Kwa sababu shauri hilo lilikuwa ni la kikatiba lilisikilizwa na majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika masijala kuu ya mahakama hiyo (Main Registry) kwa mujibu wa sheria.



Mahakama Kuu imempa ushindi mleta maombi (mwalimu Ezekiah Oluoch) kwa kutamka kwamba agizo hilo la wizara limeingilia uhuru wa kuabudu wa mleta maombi pamoja washiriki wenzake wa imani hiyo.



Mahakama pia imeeleza kwamba agizo la wanachi kufanya usafi kila jumamosi ya mwisho ya mwezi, halitatumika kwa mleta maombi pamoja na wenzake wa imani hiyo kwa kuwa kumlazimisha kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wake wa kuabudu kama unavyolindwa na katiba. Kwa maana hiyo kuanzia leo waumini wa madhehebu ya waadventista wasabato hawatashiriki kufanya usafi jumamosi ya mwisho wa mwezi kama inavyotakiwa.!


0 comments:

Copyright © 2018 iCHURCH Magazine