PAPA FRANCIS: HABARI ZA UONGO KWA KANISA NI SAWA NA ILE YA NYOKA KUMDANGANYA EVA KULA TUNDA



Papa Francis ameshutumu njia za udanganyifu miongoni mwa wale wanaosambaza habari bandia akisema kuwa kisa cha kwanza cha habari bandia kipo katika biblia wakati Eve alipohadaiwa na nyoka kula tunda lililokatazwa.

Kisa hicho kinaonyesha athari kali ambazo habari bandia zinaweza kusababisha, Papa Francis alionya katika nakala.

Francis amesema kuwa hatua hiyo ilisababisha kusambaa kwa chuki na kiburi.

Aliwataka watumizi wa mitandao ya kijamii na waandishi kutotumia njia ambazo zinaweza kusababisha migawanyiko.

Nakala hiyo kwa jina Ukweli utakuwacha huru, habari bandia na uandishi wa amani ilitolewa kabla ya kufanyika kwa siku ya mawasiliano ya kanisa hilo itakayofanyika tarehe 13 mwezi Mei, na ilikuwa mara ya kwanza Papa Francis kuandika kuhusu mada hiyo. 

Amewataka watumizi wa mitandao ya kijamii na waandishi kukabiliana na njia za udanganyifu ambazo husababisha migawanyiko.

Inajiri huku kukiwa na mjadala wa njia za kukabiliana na habari bandia katika mitandao ya kijamii na vile zitakavyoshawishi uchaguzi wa hivi karibuni, ikiwemo Marekani 2016.

''Usambazaji wa habari bandia unalenga kuendeleza malengo fulani ,kushawishi maamuzi ya kisiasa na kuhudumia maslahi ya kiuchumi'', alisema Papa Francis

Akilinganisha na ujumbe wa majaribio katika biblia, aliongezea: Lazima tufichue njia ambazo zinaweza kuitwa za udanganyifu zinazotumika na wale wanaodanganya kwa lengo la kushambulia wakati wowote na eneo lolote lile.

Alitaka kuwepo kwa elimu kuhusu ukweli ambayo itawaelimisha watu kutambua kutathmini na kuelewa habari.

Aliongezea kwamba jukumu la waandishi ambao aliwaita walinzi wa habari sio kazi pekee bali ujumbe.

Alisema kuwa hawafai kuangazia sana habari mpya bali kutathmini maswala tata yanazua mizozo.

SOURCE: BBC SWAHILI

0 comments:

Copyright © 2018 iCHURCH Magazine