KANISA KATOLIKI DRC LALAANI UTUMIAJI NGUVU WA SERIKALI
Kanisa Katoliki nchini DRC limelaani vikali utumiaji nguvu katika kuzuwia mandamano ya waumini wa kikatoliki ya kumpinga rais Joseph Kabila.
Kadinali wa Kinshasa Laurent Monsengwo amevitaja vitendo hivyo vya jeshi na polisi kuwa vya ukatili. Monsengwo ameukosowa pia utawala wa rais Joseph Kabila ambao ameuelezea kuwa usiojali raia wake na unaojirundikia mali za umma.Polisi kwa upande wake wamekanusha taarifa ya utumiaji nguvu uliozidi kiasi na kukanusha idadi ya vifo iliotolewa na wandalizi wa mandamano hayo.
Kiongozi wa kanisa Katoliki mjini Kinshasa, kadinali Laurent Monsengwo alikuwa na matamshi mazito katika kulaani kile alichoelezea kuwa ni ukatili wa maafisa wa jeshi na polisi dhidi ya wandamanaji wa kanisa katoliki.
"Kuwazuwiya waumini kutoingilia kanisani kwa ibada, wizi wa pesa na simu za waumini hao,msako waliofanyiwa na polisi na jeshi.Kuingia kwa wanajeshi hao hadi makanisani ilikuwasaka wale wanaoelezea kuwa ni waletafujo,kuwapiga risasi watu ambao hawakuwa na silaha ni vitendo vya ukatili ambavyo vinatakiwa kusitishwa haraka," kadinali Laurent Monsengwo.
Kadinali Monsengwo amewataka viongozi dhaifu kuondoka ili kuweko na amani na sheria nchini Kongo. Kwenye ujumbe wake huo aliousoma mbele ya waandishi habari, Monsengwo amehoji juu ya dhamana ya viongozi wa taifa.
"Vipi kuwapa imani viongozi wanaokeuka haki za imani ya wananchi wao ? haki hizo ambazo ni msingi wa uhuru wa na haki za binadamu kama alivyoandika baba mtakatifu Benedict wa 16," ameongeza kadinali Laurent Monsengwo.
Kadinali wa Kinshasa ameomba kuweko na uchunguzi wa kina wa machafuko hayo na wahusika kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo kanisa Katoliki halikutaja idadi ya watu waliouliwa au uharibifu uliofanywa kwenye makanisa yake. Waandalizi wa mandamano hayo ya kumpinga rais Joseph Kabila walielezea kwamba ni watu 12 waliouwawa na wengine 140 kushikiliwa na polisi.
Kwenye mkutano na waandishi habari, msemaji wa polisi alitupilia mbali madai hayo na kusema hakukuwa na mafaa ya moja kwa moja kutokana na mandamano ya waumini wa Katoliki. Kanali Pierrot Mwanamputu amesema kwamba watu watano walifariki katika mazingira tofauti na hayo ya mandamano.
"Hakukuwa na kisa hata kimoja cha mauwaji kwenye makanisa.Siku ya leo tunahakikisha kwamba watu 5 walifariki juma pili,wawili ni majangili waliotaka kuiba kwenye duka moja wapo la mtaa wa matete wakauwawa na walinzi wa duka hilo, mwengine ni mfuasi wa kundi la Kamwina Nsapu ambae alishambulia kituo cha polisi, tulipoteza pia afisa mmoja wa polisi na huko Kassai- mtu mmoja ambae ni mpiganaji wa kamwina Nsapu pia aliuliwa", amesema Kanali Pierrot Mwanamputu.
Kongamano la maskofu nchini Kongo,CENCO,limeomba utekelezaji na wa nia njema wa mkataba wa kisiasa wa mwaka 2016 ilikuweko na taratibu ya uchaguzi iliotulivu. Wandalizi wa mandamano hayo wameahidi kwamba mandamano hayo yataendelea hadi hapo rais Kabila atakapotangaza kwamba hatowania muhula wa 3 wa urais, kuachiwa huru wafungwa wa kisiasa na kufanyiwa mageuzi tume ya uchaguzi.
Afisa wa usalama akiwatawanya waandamanaji mjini Kinshasa, DRC |
0 comments: