Mwongozo wa Kutafakari na kuombea ndoto zenye MAONYO ya Mungu kuhusu HALI YA UCHUMI WAKO na Mwalimu Christopher Mwakasege


Bwana YESU asifiwe!
Nataka tujifunze mwongozo huu kwa kupata majibu ya maswali yafuatayo:

Swali la 1: Je, Mungu huwa anatumia ndoto kuonya mtu?
Jibu: Ndiyo – Mungu huwa anaweza kutumia ndoto kumpelekea mtu maonyo. Mungu aliwahi kutumia njia hii ya ndoto kuwaonya “mamajusi”. Biblia inasema: “Mamajusi wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode wakaenda zao kwao kwa njia nyingine” (Mathayo 2:2).
Tunaona pia ya kuwa, Yusufu – mume wa Mariamu, naye alionywa na Mungu kwa njia ya ndoto, kama tusomavyo katika Mathayo 2:22 hivi: “…naye akiisha kuonywa katika ndoto, akasafiri pande za Galilaya”.
Mungu akikuonya kwa njia ya ndoto, na ukapuuzia maonyo hayo, na usiyafuate, gharama inaweza ikawa kubwa sana kwako!
Ingekuwa gharama kubwa sana kama “Mamajusi” na “Yusufu”, wangepuuzia maonyo ya Mungu waliyopelekewa kwa njia ya ndoto!

Swali la 2: Kwa nini Mungu analazimika kutoa maonyo kwa watu wake juu ya hali ya uchumi wao?
Jibu: Ni kwa sababu ya uaminifu wake alionao, katika kutimiza, na kusimamia alichoahidi juu ya uchumi, kilichomo katika agano lake na wanadamu.
Baadhi ya mistari ya biblia inayotupa kupata jibu hili ni Kumbukumbu ya Torati 8:18; Zaburi 23:1, 6; Isaya 48:17 na 2 Wakorintho 8:9
Na njia mojawapo ambayo Mungu anaitumia kutoa maonyo juu ya hali ya uchumi, ni njia ya ndoto kama tusomavyo katika Mwanzo 41:1 – 7.

Swali la 3: Je, ni vitu gani ambavyo Mungu huwa anavitumia mara kwa mara, katika kutoa maonyo kwa njia ya ndoto, kuhusu hali ya uchumi wa watu wake?
Jibu: Mungu anatumia vitu vifuatavyo:
(i) Mungu anatumia picha ya vitu tunavyotumia kupata kipato, na kutunza uchumi wetu; kwa mfano – katika ndoto za wafanyakazi wa Farao alitumia KAZI zao! Soma Mwanzo 40:9 – 19. Na kwenye ndoto ya Farao (Mwanzo 41:1 – 7), alitumia vyanzo vya kipato cha uchumi wa kitaifa – ambavyo vilikuwa ni – ukulima, ufugaji na mto.
(ii) Mungu huwa pia anatumia mistari ya neno la biblia, inayohusu uchumi, na kupata kipato…ili mtu aweze kusikia asemacho kwenye ndoto. Hii ni kwa sababu “…kusikia huja kwa neno la Kristo” (Warumi 10:17). Soma pia Ayubu 33:14, 15 na Mwanzo 41: 28 – 32.
(iii) Mungu anamtumia pia Roho Mtakatifu, ili aweze kukuelimisha unachokisikia, kwenye neno linalohusika, au lililomo kwenye ndoto husika. Soma Luka 24:45
Kumbuka ya kwamba: Ndoto ni ujumbe katika picha! Picha ambayo wakati mwingine huwa inaambatana na sauti!

Swali la 4: Kwa nini kuomba peke yake hakutoshi kufuatilia maonyo ya jinsi hii kuhusu uchumi?
Jibu: Ni kwa sababu uchumi ni jambo lililomo kwenye agano, (au mapatano ya) kiushirikiano, kati ya Mungu na mwanadamu.
Ndani ya agano kuna jambo la kufanya kwa kila mshiriki wa agano! Na kwenye uchumi ni vivyo hivyo! Kuna mambo ambayo mwanadamu anayotakiwa kuyafanya pamoja na maombi, ikiwa anataka uchumi wake uwe mzuri. Na kuna mambo ambayo Mungu anatakiwa kuyafanya pia!

Swali la 5: Ni maeneo gani ambayo Mungu ameyapa kipaumbele katika kutoa maonyo kuhusu uchumi kwa njia ya ndoto?
Jibu: Baadhi ya maeneo yaliyopewa, au yanayopewa, au yatakayopewa kipaumbele kimaonyo kiuchumi ni kama yafuatayo:
(i) Mabadiliko ya nyakati za kiuchumi katika maisha yako – kama vile – ukaribu wa kifo cha mtu unayemtegemea kiuchumi; mabadiliko ya uongozi kufuatana na nyakati za cheo husika; nakadhalika
(ii) Mashambulizi toka kwa shetani, yanayolenga kuleta athari kwenye uchumi wako:
(iii) Kukwama kwa uchumi wako;
(iv) Kiwango cha ‘spidi’ ya ukuaji wako wa uchumi.
Mifano ifuatayo itakupa kuona uhusiano wa neno la Mungu la biblia, linavyoweza kukupa ufahamu juu ya ujumbe, uliomo kwenye ndoto zenye maonyo hayo:

Mfano wa 1: Ukiota kiongozi anayekuhusu amekufa - maana yake nini?
Kufuatana na Kutoka 1:6 – 14 na 2 Wafalme 4:1, ndoto kama hiyo ina maana ya kukutaarifu juu ya ujio wa kifo hicho, na mabadiliko ya maisha yako kiuchumi baada ya kifo cha kiongozi huyo.
Ndoto kama hiyo inapotoa taarifa ya kifo hicho – inamtaka aliyepewa taarifa hiyo, aombe ili Mungu awape maandalizi kwa watakaoathirika kiuchumi kwa kifo cha mtu huyo; na kuomba ikiwa ni mapenzi ya Mungu Kiongozi huyo – wa familia, au wa jamii, au wa kampuni – aongezewe miaka ya kuishi.

Mfano wa 2: Ukiota ndoto unaona sisimizi, au Siafu wamebeba chakula chao na kupeleka kwenye vichuguu vyao – maana yake ni nini?
Ndoto kama hiyo ina maana unapewa taarifa ya kuwa, mbele yako unakuja umaskini kwa sababu ya kukosa akiba. Kwa hiyo unahimizwa uweke akiba mapema. Tafsiri hii ni kufuatana na Mithali 6:6 – 11 na Mithali 30: 24, 25.

Mfano wa 3: Ukiota ndoto unaona mto uliokuwa tegemeo la uchumi umekauka – maana yake nini?
Kufuatana na 1Wafalme 17:6 – 8 ndoto kama hii maana yake: (i) Mbele yako kuna kuhama eneo ulilopo, kwa sababu ya hali ya uchumi kuwa mbaya kwako kwenye eneo hilo:
(ii) Kuna mabadiliko ya chanzo cha kipato yanakuja kwako

Mfano wa 4: Ukiota ndoto unaona ng’ombe wamekonda – maana yake nini?
Kufuatana na Mwanzo 41:3,4, 27 ndoto kama hiyo maana yake ukame na njaa vinakuja, kwa hiyo unahitajika kujiandaa, ili usije ukapata shida kiuchumi, hali hiyo itakapotokea. Lakini unaweza pia kumwomba Mungu, ili aepushe jambo hilo, ili lisitokee kama ulivyoliona kwenye ndoto yako.

Mfano wa 5: Ukiota ndoto unaona ngano au mahindi (au zao jingine) – vimekauka maana yake nini?
Ndoto kama hii ina maana kuna ukame na njaa vinakuja kwenye eneo uliloliota kwenye ndoto. Kwa ajili hiyo unahitaji kujiandaa vyema, ili usije ukapata shida hali hiyo itakapotokea; au unatakiwa ufanye maombi ili Mungu aepushe njaa na ukame visitokee kwenye eneo uliloliona kwenye ndoto yako. Hii ni kufuatana na Mwanzo 41: 6, 7, 27.

Mfano wa 6: Ukiota ndoto unaona watu wamekaa mitaani, au nyumbani saa za kazi, na hawafanyi kazi – maana yake nini?
Kufuatana na 1Mambo ya Nyakati 12:32, ndoto hiyo ina maana ya kuwa, kuna tatizo la kukosa ajira, linalokuja kwenye eneo uliloliona kwenye ndoto hiyo, kwa hiyo maandalizi yanatakiwa ili kukabiliana nalo.

Mfano wa 7: Ukiota unaona umelala wakati muda huo unatakiwa uwe unafanya kazi – maana yake nini?
Ndoto ya namna hii (i) Kufuatana na Mithali 6:9 – 11 na Mithali 24:33, 34 unaonywa juu ya tabia ya uvivu inayokuandama, ambayo inaweza ikakusababishia uchumi wako kuharibika, ikiwa hutajirekebisha mapema!
(ii) Kufuatana na Mathayo 13: 24 – 25 unapewa onyo na angalizo ya kuwa, “adui” anataka kupandikiza “magugu” kwenye eneo linalokuhusu, ili usipate “matokeo” unayotarajia.

Mfano wa 8: Ukiota ndoto unaona nyoka ameingia kwenye eneo unalopatia kipato chako – na ukaamka toka usingizini nyoka huyo akiwa hajaondoka eneo hilo – maana yake nini?
Kufuatana na Mwanzo 3:13, 23, 24 na 2Wakorintho 11:3, ndoto hiyo maana yake, unapewa taarifa ya kuwa usipotubia, au usipotubu juu ya udanganyifu na hila zilizopo kwenye eneo unalopatia kipato (hata kama si wewe unahusika), ujue utafukuzwa, au utatafutiwa sababu ya kukufanya uondoke kwenye eneo hilo!

Naamini mifano hii inatosha kukupa picha, inayokusaidia kujua namna ya kuunganisha neno la Mungu (biblia), na tafsiri ya ndoto uliyoota, yenye maonyo kwako, juu ya hali ya uchumi wako.
Mungu azidi kukubariki sana!

0 comments:

Copyright © 2018 iCHURCH Magazine