ASKOFU KAKOBE AELEZA ALIVYOHOJIWA NA TRA

askofu kakobe

Dar es Salaam. 
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amewaelezea waumini wake jinsi alivyohojiwa na timu mbili zilizoundwa kwa nyakati tofauti na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Askofu Kakobe, ambaye ameingia kwenye mgogoro na mamlaka za nchi tangu aeleze kuwa ana utajiri mkubwa, alisema hayo wakati wa ibada iliyofanyika katika kanisa lake lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya pili kuzungumzia sakata hilo kwa waumini wake tangu Desemba 31 mwaka jana.

Hata hivyo, Kakobe alisema kutoa mrejesho huo hakuwazuia TRA kueleza waliyobaini, lakini amesema ameona azungumze mapema na waumini wake kwa kuwa ndio watoa sadaka na wana haki kwa asilimia 100 kujua kinachoendelea kanisani kwao.

“Baada ya kuleta barua, Januari 2, kiongozi wa tume iliyoundwa awali na kikosi chake walifika na tuliwapa ushirikiano. Nilikuwa nao katika ofisi ya kiuchungaji kwa mahojiano, walikuwa na karatasi za maswali na majibu waliyaandika,” alisema.

“Waliuliza kuhusu utajiri wangu, niliwaambia nina nyumba moja tu duniani ipo Kijitonyama niliijenga kwa gharama ya Sh2 milioni na kiwanja nilinunua Sh30,000. Ni nyumba ya kawaida na ipo katika mtaa wa kawaida uitwao kwa Kakobe. Utafuteni mtaiona nyumba yangu.”

Askofu Kakobe alisema aliwaeleza wazi kuwa ana waumini wake ambao hawakuridhishwa na anapoishi, hivyo walitamani awe na sehemu nzuri itakayoweza kufaa kwa ajili ya wageni wa kimataifa wanaoweza kuwatembelea. Alisema walimshirikisha hilo na walijenga eneo jingine kwa michango yao miaka 10 iliyopita.

Alisema suala la akaunti za kanisa aliliweka wazi na kuwaambia kuwa kuna akaunti benki ya NBC na akaunti ya mfuko wa kitaifa wa FGBF iliyopo pia NBC Meru, Arusha.

“Niliwaambia wazi mimi wala mke wangu hatuna akaunti benki. Binafsi sina mradi wowote, sina shamba, sina kuku hata mmoja, paka na wala panya niliyefuga. Niliwaambia hata kanisa hatuna mradi wowote wa kiuchumi na hivi ndivyo tunavyoishi,” alisema.

“Mmoja akaniuliza kwa nini hamna mradi wa kiuchumi, nilimweleza huo ni wito wetu. Wakatoa karatasi moja ya kumbukumbu za TRA wakasema kuna shule moja inaitwa Full Gospel si yenu? Nikasema hatuijui ila ni neno ambalo linatumika kote duniani. Mkifuatilia vizuri mtajua wenye shule ni ya kina nani.”

Alisema walimuuliza iwapo ameajiri watu kanisani, akasema kuna watumishi zaidi ya 1,000 ambao hawalipwi wanafanya kazi ya Mungu na huo ndiyo mfumo wa kanisa.

Alisema walimuuliza kuhusu ukusanyaji wa sadaka, maisha yake bila ya kuwa na mradi wowote na baadaye waliitwa wakusanyaji sadaka kwa mahojiano zaidi.

“Wakauliza kutoka kwa hicho kikosi ‘bahasha za maombi maalumu ambazo huelekezwa kwa mchungaji zinakuwa nzito sana’, wakasema zinakuwa za kawaida tu. Wakaniambia kwa uzoefu wako kiasi gani huwa kinapatikana kwa mwezi, nikawaambia hufika hata Sh5 milioni lakini wakati mwingine kinaweza kwenda chini.”

Alisema baada ya hapo walihojiwa watoto na mke wake na kijana wake mmoja na majibu yakawa yaleyale. Alisema walichukua baadhi ya kompyuta na nyaraka muhimu kwa ajili ya uchunguzi na baadaye walitoa maoni yao.

“Kilichofuatia ndicho kilichonifanya nitoe mrejesho kabla ya TRA. Yule kiongozi niliyekabidhiwa na TRA alitoa ripoti inayoonyesha sina miradi wala vyanzo vya fedha, kinachosalia ni sadaka na wao hawahusiki nazo,” alisema Kakobe.

“Baada ya kiongozi huyo kutoa ripoti hiyo, aliondolewa katika hiyo kazi na hivi tunavyozungumza amepelekwa mkoani. Nikasema sasa nitamwaga mboga leo, nikasema hapa kuna hila, nitaitungua ndege kabla haijapaa.”

Askofu Kakobe alisema baada ya kiongozi huyo kutimuliwa ameletwa kiongozi mwingine na kazi imeanza upya, “Wamekwenda nyumbani kwangu wamekagua chumba kwa chumba, vyumba vyote nguo za wanangu, mke wangu; wanachambua nguo mojamoja yaani wanasagula kama mtumbani. Wamekuja ofisini hivyohivyo. Wameenda kwa viongozi wangu wamefanya hivyohivyo,” alisema.
Alisema wamehoji wapi anapeleka fedha na kuwapa mrejesho kuhusu safari zake za ndani na nje ya nchi lakini hawajaridhika.

“TRA sasa ipo ndani ya sadaka. Hii ni TRA kweli? au kuna jambo? Mimi leo nimemwaga mboga, hata (Askofu Josephat) Gwajima aliwahi kutoa mrejesho. Sasa Gwajima na Kakobe ni mapacha. Walikuja ofisini wanakagua chumba kimoja mara kingine nikasema watumishi tuwe macho wasijekutuwekea bangi,” alisema.

Aidha katika hatua nyingine, Askofu Kakobe aliwataka watumishi wa TRA kufuata utaratibu na ikiwa wataanza kukusanya sadaka basi wakusanye makanisa yote.
Alitoa onyo kwa watumishi hao na kusema wanamchonganisha Rais John Magufuli na wananchi wake kwa kuwa haamini kama wametumwa.

“Ninavyomjua Rais John Magufuli ana hofu ya Mungu. Nalikumbuka neno lake la ‘mniombee nisiwe na kiburi’ na sijayasahau. Leo kama anatuma TRA wachunguze sadaka sina imani hiyo. Tunajua kuna watu siku hizi wanatafuta kiki, wanatafuta kupanda vyeo, nakushauri Rais wanaotafuta vyeo kwa staili hii wageukie na uwatumbue,” alisema.

SORCE: MWANANCHI
_________________________________________________________________________________

0 comments:

Copyright © 2018 iCHURCH Magazine