SERIKALI HAIMTAMBUI NA YAMUONYA ANAYEJIITA NABII TITO


Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Sheria wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Marlin Komba amesema hamtambui mtu anayejiita nabii Tito na kwamba hajasajili kanisa lake katika ofisi ya msajili wa taasisi za dini.

Komba amesema Serikali imeona vitendo anavyovifanya ‘nabii’ huyo kupitia mitandao ya kijamii na imeanza kuchukua hatua.

“Ninachoweza kusema ni kwamba hakuna mtu anayezuiwa kuongea hapa nchini, mwache aongee anavyoweza ila Serikali imeshaona anachokifanya na yanayoendelea mitandaoni na hatua zinachukuliwa dhidi yake,” amesema Komba.

Kwa upande wao viongozi wa dini wameonyeshwa kukerwa na kulaani vitendo anavyovifanya mtu huyo anayejiita nabii na kusisitiza kuwa hakuna dini inayoruhusu hayo.

Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chediel Lwiza amesema kwa vitendo anavyofanya mtu huyo hapaswi kujiita mtumishi wa Mungu.
"nabii Tito akifundisha Pombe ni dawa ya
UKIMWI...

“Huyo hawezi kuwa mtumishi wa Mungu na wala hafanyi huduma ya kanisa ni vyema watu kama hawa wafuatiliwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Natumaini Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ndani yake ina ofisi ya msajili wa taasisi za dini itafanya kazi yake.”

Lwiza ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania kwenda kwenye makanisa ya kweli yanayozingatia neno la Mungu.

Amesema, “Hakuna sababu ya kutangatanga, Watanzania mkasali kwenye makanisa yanayotambulika na yanayosimamia na kufundisha neno la Mungu. Kuhangaika ndiko kunakowafanya wengine waangukie kwa watu kama hao. Wapo wanaojaribu kupotosha neno la Mungu lakini ukweli ni kwamba neno la Mungu halipotoshwi.”

Hilo limeungwa mkono na Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Rajab Katimba ambaye amesisitiza Serikali na viongozi wa dini kuingilia kati suala hilo.

Amesema hakuna kitabu chochote cha dini kinachohamasisha ulevi na ukosefu wa maadili.

“Hilo suala linakwenda tofauti na dini na mila na desturi zetu pia. Dini zinatakiwa kuleta amani na kuhamasisha watu waheshimiane si kuzungumza mambo yanayokiuka maadili yetu. Naona ipo haja ya viongozi wa dini na Serikali kuingilia suala hili na waende mbali zaidi kwa kuongea naye huenda hafahamu anachokifanya.”

0 comments:

Copyright © 2018 iCHURCH Magazine